Abstract
Mwingilianomatini ni mbinu, stadi ama taaluma na mwongozo wa uchunguzi wa matini kisayansi, hususani kazi za kisanaa na zisizo za kisanaa ili kubaini kuwepo kwa athari ya uchopekaji ama usemezano; yaani kufanana kifani, kimaudhui na kimbinu kati ya matini moja na nyingine. Ufanano huo huweza kuwa wa moja kwa moja au kuwapo kwa ukaribiano. Mwingiliano huo hutambulika pia kama mwangwi. Inaaminika kwamba, mwingilianomatini ni miongoni mwa mbinu kongwe za kiutunzi, ilhali kiuhakiki inaonekana bado ngeni, haijashughulikiwa sana katika uga wa fasihi na sanaa ya Kiswahili. Kwa mantiki hiyo, makala haya yatasaidia kuongeza maandiko ya Kiswahili yaliyoshughulikia eneo la uhakiki kupitia nadharia ya mwingilianomatini ili kubaini mwingilianomatini uliopo katika matini, kwa mfano tamthilia ya Utangamano Wetu Ushindi Wetu. Matokeo ya uchambuzi yamebaini kuwapo kwa mwingilianomatini mwingi unaofungamana na historia ya makuzi na malezi ya mwandishi kidini (kiroho), kimwili (kiutamaduni na kimaadili), kijamii na kitaaluma – kwa namna moja ama nyingine. Sehemu ya matokeo hayo ndiyo inayobeba makala haya. Hivyo basi, makala yanawasilisha mwingilianomatini kati ya tamthilia teule ya Utangamano Wetu Ushindi Wetu na maandiko kutoka vitabu vitakatifu, majazi katika uteuzi na uumbaji wa wahusika, mwangwi wa kifalsafa, anwani za sura au ploti, na mithiolojia ya kiishara.
How to cite
Furaha J Masatu, Venancia F Hyera, Osmunda R Ndunguru, Aneth K Ponera (2020). Mwingilianomatini katika Tamthilia ya Utangamano Wetu Ushindi Wetu (2017) ya Anitha E. Mgimba. East African Journal of Swahili Studies. https://doi.org/10.37284/eajss.2.2.217
Republished on Discussion Research from the global Crossref scholarly index with full credit to the original authors and East African Nature and Science Organization. Licence: http://creativecommons.org/licenses/by/4.0
