Abstract
Makala yanawasilisha sehemu ya uchunguzi uliolenga kubaini na kufafanua mafunzo yanayopatikana katika Ushairi Andishi wa Kiswahili wa kipindi hiki cha utandawazi kwa kuangazia diwani ya Kimya! (2020) ya Rehema N. Mbwambo. Uchunguzi huu umeongozwa na nadharia ya uhakiki wa kazi za fasihi ijulikanayo kama Uhistoria Mpya. Huu ni msingi mpya wa kihakiki ambao haujatumika sana katika kuhakiki kazi za kifasihi. Uhakiki unaoongozwa na nadharia hii ya Uhistoria Mpya, humsaidia mwanafunzi kujenga uwezo na maarifa ya kutambua sababu, uzito, malengo na aina ya uhakiki uliofanyika. Kwa kuzingatia ukweli huu, uchambuzi wa kipindi hiki cha utandawazi ni lazima uanze kuwazoesha watunzi, walimu na wanafunzi kujikita katika utunzi na uchambuzi wa kazi za kifasihi kwa kutumia nadharia teule badala ya kutunga na, au kuhakiki kazi kimkururo yaani, utunzi au uhakiki jumuishi usiokuwa na dira mahususi kama sehemu muhimu ya kwenda na wakati. Matumizi ya nadharia teule ya uhakiki yanatusaidia kujua iwapo kazi bunilizi za fasihi zinazoingia sokoni zinaakisi mahitaji ya jamii ya wasomaji wa sasa ama la. Kwa sababu, kumekuwapo madai ya kwamba, ari ya usomaji wa kazi bunilizi za Kiswahili inazidi kushuka miongoni mwa walaji wa kazi bunilizi za Kiswahili hasa nchini Tanzania huku moja ya sababu zinazotajwa ni baadhi ya watunzi na wahakiki kukosa weledi, ubunifu, ubora na kushindwa kuisoma jamii inataka nini. Hofu yetu ni kuwa, kama kweli wasomaji wanazidi kupoteza hamu ya kupenda kusoma kazi bunilizi za Kiswahili kwa sababu kadhaa ikiwemo ubunifu na saikolojia, maana yake kwa siku za usoni, pale ambapo watunzi nguli watakapokuwa wametoweka katika uso wa dunia, fasihi ya Kiswahili nayo itakuwa imeanguka kisanaa na kibiashara. Ndiposa, tukaonelea tufanye uchunguzi katika diwani mpya iliyoandikwa na mwandishi chipukizi kwa lengo la kuona iwapo nayo ni sehemu ya kazi bunilizi za Kiswahili zinazochangia anguko la ukuaji na ustawi wa Fasihi ya Kiswahili ama la.
How to cite
Furaha J Masatu, Venancia F Hyera, Osmunda R Ndunguru, Aneth K Ponera (2020). Mafunzo Yanayotawala Ushairi Andishi wa Kiswahili wa Kipindi cha Utandawazi: Mifano Kutoka Diwani ya Kimya! (2020) ya Rehema N. Mbwambo. East African Journal of Swahili Studies. https://doi.org/10.37284/eajss.2.2.199
Republished on Discussion Research from the global Crossref scholarly index with full credit to the original authors and East African Nature and Science Organization. Licence: http://creativecommons.org/licenses/by/4.0
